Benki ya Dunia yapingana na takwimu za ukuaji wa uchumi za serikali

0
37

Benki ya Dunia (WB) imesema kuwa uchumi wa Tanzania ulikua kwa asilimia 5.2 mwaka 2018, takwimu ambazo zinapinga na zile zilizotolewa na serikali ambazo zinaonesha kuwa kwa mwaka huo uchumi ulikua kwa asilimia 7.

Mbali na hilo taasisi hiyo kubwa ya kifedha dunia imesema kuwa kwa mwaka 2019 uchumi wa Tanzania utakua kwa asilimia 5.4, tofauti na takwimu za serikali zilizotolewa na Wizara ya Fedha na Mipango ambazo zinaainisha kuwa kwa mwaka huu, uchumi utakua kwa kasi ya asilimia 7.1

Takwimu hizo ya Benki ya Dunia kuhusu ukuaji wa uchumi wa Tanzania ni sehemu ya ripoti ya benki hiyo kuhusu hali ya uchumi wa Tanzania iliyotolewa Julai 18 jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Dk Albina Chuwa amepinga takwimu hizo za WB, huku akihoji uhalali wa taarifa zilizotumika kupata takwimu hizo.

Wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo, WB imesema kuwa takwimu zilizowezesha kupatikana kwa makadirio hayo zimetoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Dk Chuwa amesema ofisi hiyo inaunga mkono takwimu za ukuaji wa uchumi zilizotolewa na serikali.

WB imesema ipo tayari kuketi na TRA, BoT na NBS wapitie kwa pamoja ripoti hiyo na kubaini kama kuna sehemu yenye mkanganyiko ili iweze kuondolewa.

Hii ni mara ya pili kwa mashirika ya kimataifa ya fedha kupingana na takwimu za ukuaji wa uchumi zinazotolewa na serikali, ambapo Aprili mwaka huu, Shirika la Fedha Duniani (IMF) lilipunguza makadirio ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania hadi asilimia 4, takwimu ambazo zilipingwa na serikali.

Ripoti ya IMF ambayo ilivuja ilionesha kuwa uchumi wa Tanzania kwa mwaka 2020 utakua kwa asilimia 4.2.

Kupata ripoti ya WB bonyeza hapa

Send this to a friend