Benki ya NMB na Kampuni ya Agricom Africa, wamewahakikishia wakulima nchini, kwamba ushirikiano baina ya taasisi hizo ndio mkombozi wa Sekta ya Kilimo, hivyo kuwataka kuchangamkia fursa za mikopo nafuu ya pesa, zana za kilimo hususani matrekta, ‘power tillers’ na pembejeo ili kufanya kilimo chenye tija.
Hayo yamesemwa katika viwanja vya maonesho ya Kitaifa ya Kilimo ya Nane Nane jijini Mbeya na Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa NMB – Nsolo Mlozi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Agricom Africa – Bw. Alex Duffar.
Akizungumza,Mlozi alisema NMB na Agricom wanafahamu kwamba Kilimo cha Tanzania kinahitaji miundombinu, pembejeo na zana bora na za kisasa, eneo ambalo wamejipanga vya kutosha kuwafikia wakulima wote – Bara na Zanzibar, hasa vijana na kinamama ambao ndio nguvu ya Taifa katika kilimo.
Alifafanua zaidi kuwa NMB wana bajeti ya mabilioni ya mikopo na mtandao mpana unaojumuisha matawi 229 kote Tanzania, huku washirika wao Agricom nao wakiwa na matawi zaidi ya 12 kwenye Kanda mbalimbali, hivyo, wana uhakika kuwa wateja wao wanakuwa na Kilimo chenye tija na biashara ya sekta hii kwa ujumla wake itaenda vizuri.
Bw. Nsolo aliwaomba wakulima waende NMB na Agricom sio tu kupata mikopo ya pesa, zana, mashine na pembejeo bora, bali pia wapate ushauri – kwani wanaenda shambani moja kwa moja kumshauri mahitaji mazuri kwake, kisha atakopa kwa riba nafuu ya asilimia 9 kwa mwaka na marejesho ni kulingana na hitaji na msimu. Lakini sio hivyo tu, wakulima watakaokopa mashine, zana za kilimo ama pembejeo watalazimika kuwa na asilimia 20 tu ya malipo, na NMB itamlipia asilimia 80, kisha mkopaji kuwa huru kulipia marejesho yake mpaka miezi 36 kuresha mkopo huo.
Naye Duffar, alisema ukubwa wa mtandao mpana wa matawi ya NMB na mafanikio yao kibiashara, kwa pamoja wanadhamiria kuboresha Kilimo nchini -ukizingatia ubora wa zana za Agricom kutoka Kampuni tanzu bobezi za utengenezaji mashine za kilimo, unawahakikishia wakulima suluhishi ambazo hawawezi kuzipata kwingine.
NMB wamejipanga kuongeza tija kwenye kilimo, ambayo wanaitazama kama Sekta ya Kimkakati itakayonyanyua uchumi wa mdau na mkulima mmoja mmoja wa mnyororo huo wa thamani na Taifa kwa ujumla kama kitafanywa kisasa.