Benki ya NMB imekamilisha zoezi la kuunganisha mfumo wake mkuu wa kibenki na Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ikiwa ni utekelezaji wa sehemu ya dhamira ya benki hiyo kuimarisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wanafunzi katika vyuo vikuu kupata bidhaa za kibenki zenye hali ya juu ya usalama, ufanisi na uvumbuzi.
Akizungumza wakati wa kongamano lililofanyika jijini Dar es Salaam jana lililoandaliwa na Bodi ya Mikopo na kuwakutanisha wadau mbalimbali wa elimu chini, Afisa Mkuu wa Wateja Binafsi wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi alisema mfumo huo kwa kiwango kikubwa umerahisisha utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
“Wanafunzi sasa wataweza kufurahia huduma za kibenki bila matatizo baada ya kuunganishwa kwa mfumo mkuu wa benki ya NMB na Bodi ya Mikopo. Muunganisho huu utahakikisha kuwa mikopo sasa inatolewa kwa wanafunzi kwa haraka na kwa urahisi zaidi,” Mponzi alisema.
Aliwataka wanafunzi wa vyuo vikuu kufungua akaunti na benki yake ilikunufaika na faida lukuki zikiwemo mikopo ya papo kwa papo yenye masharti nafuu kuanzia shilingi elfu moja hadi shilingi laki 5.
Mponzi wakati wa kongamano hilo alisisitiza dhamira ya benki hiyo kuendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali pamoja na taasisi za elimunchini ili kusaidia maendeleo ya sekta ya elimu kuanzia ngazi ya chini.
“Sekta ya elimu ni miongoni mwa vipaumbele vyetu muhimu. Ili kusisitiza dhamira yetu ya kusaidia elimu ya juu, mwaka jana tulitenga mikopo ya shilingi bilioni 200 kwa wanafunzi wa vyuo vikuu kufuatia majadiliano ya karibu na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi,” Mponzi alisema.
Aliongeza, “Wanafunzi wanaweza kuomba mikopo kuanzia shilingi laki mbili hadi hadi shilingi milioni 10 kwa riba nafuu ya asilimia 9 tu.”
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Dk.Bill Kiwia wakati wa hafla hiyo alisema lengo la kongamano hilo ni kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali wanaohusika na utendaji wa utoaji wa fedha kwa taasisi yake.
Alisema kuwa bodi hiyo kwa sasa inawafikia zaidi ya wanafunzi laki mbili wenye uhitaji lakini tayari imepanga mipango ya kuwafikia wanafunzi wengi zaidi na kuongeza kuwa hata hivyo itategemea upatikanaji wa rasilimali fedha.
“Hatujaridhishwa na hali ya sasa kwa sababu mahitaji ni makubwa kuliko rasilimali zilizopo. Bado tunatafuta rasilimali fedha mbadala ili kuwafikia wanafunzi wengi zaidi,” alisisitiza.
Aliwataka wanufaika wa mikopo ya bodi yake kuhakikisha wanarejesha mikopo yao kwa wakati ili kuiwezesha taasisi yake kujiendesha kwa ufanisi kwa manufaa ya wanafunzi wengi wenye uhitaji.