Benki ya NMB imepata idhini kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana (CSMA) kuwa wakala wa madalali wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE).
Kupitia idhini hiyo wananchi sasa wataweza kuuza na kununua hisa na hatifungani kupitia mtandao mpana wa matawi 231 wa Benki ya NMB yaliyopo nchi nzima.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini Mkataba wa Mawasiliano baina (MoU) baina ya Benki ya NMB na kampuni ya udalali wa hisa ya Orbit Securities, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna huku akiinukuu ripoti ya Finscope ya mwaka 2023 alisema asilimia 0.5 tu ya Watanzania wanatumia soko la mitaji kuwekeza.
“Nina imani kwamba makubaliano haya ya kimkakati yatafungua ukurasa mpya siyo tu kwa Kampuniu ya Orbit Securities bali na madalali wengine wa Soko la Hisa la Dar es Salaam. Natumia nafasi hii kuwakaribisha madalali wengine kuja kuingia makubaliano nasi ili kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kutumia masoko ya mitaji,” alisema.
Alitoa shukrani kwa Benki Kuu ya Tanzania na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kwa kutoa idhini kwa benki yake huku akisistiza kuwa hatua hiyo inaonyesha imani kubwa kwa benki yake.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Orbit Securities, Godfrey Gabriel wakati wa hafla hiyo alisema, “Hii ni siku muhimu na ushirikiano huu utafungua milango kwa watu binafsi na wafanyabiashara kushiriki katika masoko ya mitaji kwa urahisi zaidi.”
Gabriel aliongeza kuwa makubaliano haya yanalenga kuunga mkono mpango wa maendeleo ya sekta ya fedha pamoja na sekta ya mitaji na dhamana ili kufanikisha lengo la ujumuishaji wa kifadha unaolenga kuongeza ushiriki wa Watanzania katika soko la mitaji na dhamana kufikia asilimia 5.
“Makubaliano yetu na Benki ya NMB yatarahisisha fursa za uwekezaji. Tunatoa shukrani kwa Benki Kuu ya Tanzania kwa kutoa idhini ya ushirikiano huu na Benki ya NMB,” alisema.
Naye Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) Mary Mniwasa katika hafla hiyo alisema, “Siku ya leo ni siku muhimu na ya kipekee katika soko la mitaji. Kwa kweli, hatua kama hii tumekuwa tukisubiri kwa miaka mingi sana ukweli madalali wetu wengi bado ni wadogo na hawana mtandao mkubwa.”
Mniwasa alisema kupitia ushirikiano huo mpya wa Benki ya NMB na Kampuni ya Orbit Securities, soko la hisa sasa litafikiwa kuirahisi zaidi kupitia mtandao mpana wa Benki ya NMB.
“Natoa pongezi kwa uongozi wa Benki ya NMB pamoja na kampuni ya Orbit Securities kwa kufungua ukrasa mpya wa ushirikiano. Ni matumaini yangu kuwa ushirikano huu utaongeza uwekezaji wa tija katika Soko la Hisa la Dar es Salaam.”
Aidha Mniwasa aliipongeza Benki ya NMB kwa uthubutu wake wa kuorodhesha kwa hatifungani yake ya Jamii Bond katika Soko la Hisa la London (LSE) siku chache zilizopita.
“Kwa kuorodhesha hati fungani katika masoko makubwa kama Soko la Hisa ya London na Soko la Hisa la Luxembourg, NMB inaendelea kupeperusha bendera ya nchi yetu vyema,” alisema.