Biashara 7 za kuanzisha bila kuwa na mtaji wa pesa

0
54

Ukosefu wa ajira ni changamoto kubwa kwa vijana wengi nchini. Baadhi wameshindwa kujiajiri kwa kigezo kuwa hakuna mitaji (pesa) ya kuanzia biashara.

Kutokuwa na mtaji haimaanishi kuwa huwezi kuanzisha biashara, kwani zipo baadhi ya biashara unazoweza kufanya bila kuwa na mtaji wa pesa. Hizi ni baadhi ya biashara hizo;

Kutoa Huduma za Kukodisha

Kama unamiliki vitu kama vifaa vya elektroniki, vifaa vya michezo, au hata mavazi, unaweza kutoa huduma za kukodisha. Hii inaweza kuwa njia nzuri ya kuanza bila kununua vitu vipya.

Usafishaji wa Nyumba na Bustani

Huduma hii inaweza kuanzishwa kwa kutumia vifaa unavyomiliki nyumbani. Unaweza kutoa huduma za usafishaji wa nyumba au bustani kwa kuanza na majirani zako.

Kufundisha ujuzi

Ikiwa wewe ni mzungumzaji mzuri wa lugha ya Kiingereza au lugha nyingine za kigeni unaweza kuanza kufundisha lugha mtandaoni au kutoa kozi ya ujuzi fulani ulionao kama njia ya kupata pesa. Unaweza kuwa mmiliki wa biashara ya kufundisha au kuwa mshirika na majukwaa mbalimbali ya mafunzo ili kutoa huduma zako.

Kuandaa hafla (Event planning)

Watu wengi hupata msongo wa mawazo linapokuja suala la uandaaji wa sherehe, unaweza ukatoa huduma hiyo pasipokuwa na mtaji wowote, utakachofanya ni kutumia bajeti yao kuandaa kila kitu kinachohitajika na kisha utalipwa kwa kazi hiyo.

Kuwa Mtafsiri

Huduma za utafsiri zinaweza kutolewa ana kwa ana. Kuna njia nyingi za kuanzisha biashara ya utafsiri kulingana na kiwango chako cha ujuzi na muda gani ulionao kwa wateja duniani kote.

Uangalizi wa watoto

Unaweza kutunza watoto pale wazazi wao wanapokuwa wameenda kazini. Huhitaji kuwa na mtaji kuanza biashara hiyo, cha muhimu zaidi ni umakini wa hali ya juu kwa watoto.

Kuuza bidhaa mtandaoni

Unaweza kuuza bidhaa mbalimbali kama simu, nguo, kompyuta na vitu vingine mtandaoni bila kuwa na mtaji. Cha muhimu ni kuingia makubaliano na maduka yanayouza bidhaa hizo na kupewa bei ya bidhaa kisha unaweza kuuza kwa bei utakayoipanga wewe.