Biashara kati ya Tanzania na Kenya imekua kufikia TZS trilioni 2.1 kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2021, Benki Kuu ya Kenya imeeleza.
Katika kipindi tajwa, mauzo ya Tanzania nchini Kenya yalikuwa TZS trilioni 1.16 huku mauzo ya Kenya nchini Tanzania yakiwa TZS bilioni 935.03, takwimu zikionesha kuwa Tanzania inanufaika zaidi kwa kuendelea kukua kwa kiwango cha mauzo tangu mwaka jana.
“Mazungumzo yaliyoanzishwa baina ya viongozi wa Tanzania na Kenya yamekuwa kichocheo kikubwa cha kukua kwa takwimu kwa biashara zinazovuka mpaka,” amesema Kevit Desai ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na Maendeleo ya Kanda.
Tanzania imeuza zaidi nchini Kenya nafaka, mbao, mboga za majani, wakati Kenya ikiuza zaidi sabuni, chuma na dawa.
Mwaka 2021 Tanzania iliuza zaidi bidhaa zake Kenya, Rwanda, Uganda na Burundi.
Katika mazungumzo yaliyofanyika kati ya Rais Samia Suluhu Hassan na Rais Uhuru Kenyatta yaliweza kuondoa vikwazo vya biashara visivyo vya kodi ambavyo awali vilikuwa vikikwamisha ukuaji wa biashara.
“Kituo cha pamoja za Taveta/Holili kilipitisha malori ya mizigo 33,000 mwaka 2021, ongezeko la asilimia 73 kutoka malori 19,000 yaliyopita mwaka 2021,” amesema John Kalisa, Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Biashara la Afrika Mashariki.
Kwa upande wa Namanga, Meneja kituo wa Mamlaka ya Mapato Kenya, Joseph Moywaywa amesema kuwa malori 250 yalikuwa yakipita kila siku, mengi kati ya hayo kutoka Tanzania kuingia Kenya