Bibi anyonga kichanga cha siku moja kwa madai ya ugumu wa maisha

0
45

Jeshi la Polisi mkoani Kigoma linamshikilia Lenita Asheri (54) kwa tuhuma za kuhusika na kifo cha mjukuu wake mwenye umri wa siku moja, akidaiwa kutenda kosa hilo kutokana na ugumu wa maisha.

Akizungumza na vyombo vya habari Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, James Manyama amesema mtuhumiwa alifanya tukio hilo Aprili 9 mwaka huu katika Kijiji cha Uvinza Wilaya ya Uvinza  Mkoani Kigoma, baada ya binti yake Penina Yekonia (20) mwenye matatizo ya akili kujifungua, na kisha bibi huyo kukinyonga kichanga  hicho na kukitupa chooni.

Aidha, inadaiwa kuwa Penina aliendelea kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua na ndipo mtuhumiwa alipoamua kumpeleka kituo cha Afya Uvinza kwa ajili ya matibabu.

Kamanda ameeleza kuwa baada ya binti huyo kufikishwa kituo cha afya, mhudumu wa kituo hicho Osward Mbara(34) alimkagua na kugundua kuwa amejifungua na ndipo muuguzi alitoa taarifa Polisi kwa uchunguzi.

Baada ya Polisi kufanya ukaguzi nyumbani kwa mtuhumiwa walikuta nguo zenye damu, walipomhoji zaidi mtuhumiwa alikiri kuwa msichana huyo alijifungua lakini wamemnyonga mtoto na kumtumbukiza chooni, kisha polisi walifukua na kukuta mwili kichanga hicho.

Hata hivyo msichana huyo alijifungua mtoto mwingine akiwa katika kituo cha Afya Uvinza, polisi kwa kushirikiana na Idara ya Ustawi wa jamii wanashughulikia mipango ya kumpeleka mtoto kituo cha kutunza Watoto cha Matyazo.

Send this to a friend