
Mwanamke mmoja wa makamo, Regina Munyoki maarufu kama Big Mama, amefikishwa katika Mahakama ya Mombasa nchini Kenya akikabiliwa na mashitaka ya kusambaza picha za ngono za watoto na utakatishaji wa fedha.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Gladys Olimo, Regina alishtakiwa kwa kusambaza picha chafu za watoto wenye umri wa miaka 4, 8 na 14, kupitia majukwaa ya kidijitali kama WhatsApp, Microsoft Teams, Telegram, na tovuti ya ngono.
Makosa hayo yanadaiwa kufanywa kati ya Januari 1, 2024 hadi Juni 1, 2025 katika maeneo tofauti nchini humo. Ripoti ya mashtaka inasema alitumia simu yake ya mkononi kupakia picha hizo mtandaoni.
Regina alikana mashtaka hayo na alikataliwa dhamana, akisubiri uamuzi wa maombi ya dhamana wiki ijayo.
Wakili Mkuu wa Serikali Breda Ogada alipinga kuachiwa kwake kwa dhamana, akisema makosa hayo ni makubwa na yanahatarisha usalama wa watoto. Akiongeza kuwa watoto hao wanahitaji ulinzi na msaada wa kisaikolojia.







