Bilioni 770 kutumika kusambaza umeme vijijini, mashuleni na vituo vya afya

0
46

Jitihada za Rais Samia Suluhu kusambaza umeme vijijini zinaendelea kuimarika baada ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Dunia imetoa fedha zaidi ya TZS bilioni 770 (Dola za Kimarekani Milioni 335) kusaidia juhudi za Serikali ya Tanzania kutimiza lengo lake.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya Benki ya Dunia (WB) kuridhishwa na kasi ya Tanzania katika kusambaza umeme vijijini ikiwa ni moja ya nchi zenye kasi kubwa zaidi katika kusambaza umeme kwa watu wake kwa Bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Umeme sasa hivi kwa mwanachi sio anasa bali ni lazima na ndiyo maana Serikali tunakopa kupeleka umeme vijijini,” alisema Rais Samia Suluhu katika moja ya hotuba zake akieleza azma yake ya kuhakikisha vijiji vyote vinapata umeme.

Akiwasilisha bajeti bunge Waziri wa Nishati, January Makamba alisema katika mwaka wa fedha 2022/23, Serikali inakusudia kuendelea na kazi ya kusambaza umeme katika vijiji 3,917 ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo muhimu, ili kupelekea vijiji vyote 12,345 vya Tanzania Bara kuwa vimefikiwa na huduma za umeme ifikapo mwaka 2024.

Kupitia fedha hizo za WB, zaidi ya maunganisho mapya ya umeme 1,000,000 ikiwemo taasisi za elimu 8,500 na taasisi za afya 2,500 yatafanyika pamoja na kutoa fursa ya nishati mbadala na salama ya kupikia kwa maeneo ya vijijini.

Mpango huu una manufaa makubwa kwa Watanzania kwani ni sehemu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kupunguza matumizi ya kuni, mkaa, mabaki ya mazao na vinyesi vya wanyama kama chanzo cha nishati kinachotegemewa na asilimia 85 ya wananchi.

Aidha, upatikanaji wa umeme vijijini utaimarisha utoaji wa huduma za kijamii (maji, elimu, afya), utafungua fursa mpya za kibiashara na kukuza zilizopo, na kupunguza vifo vya Watanzania vitakanavyo na moshi wa kupikia ambapo takwimu za sasa zinaonesha ni vifo 33,000 kila mwaka.

Send this to a friend