Binti amshitaki mchumba wake mahakamani kwa kuchelewa kumuoa

0
39

Mwanamke raia wa Zambia amemshitaki mchumba wake kwa madai kuwa amesubiri kwa miaka nane amuoe, lakini bado ndoto hiyo haijafanikiwa, gazeti la Sunday Times limeripoti.

Getrude Ngoma (26) anayeishi katika Mji wa Ndola, mkoani Copperbelt ameiambia mahakama kwamba Herbert Salaliki (28) amechukua muda mrefu sana kumuoa licha ya kuwa mwanaume huyo aliahidi kufanya hivyo.

Bi. Ngoma ameeleza zaidi kuwa licha ya kuwa na mtoto na Salaiki na mwanaime huyo kulipa mahari, yeye bado anaishi na wazazi wake badala ya kuishi na mchumba wake.

“Mheshimiwa, mwanaume huyu hajawahi kudhamiria ndio maana nimemleta mahakamani kwa sababu nahitaji kujua nini kinaendelea na hatima yangu na yeye ni ipi,” ameiambia mahakama huku akimtuhumu mwanaume huyo kuwa na uhusiano na mwanamke mwingine.

Kwa upande wa utetezi, Salaliki ameiambia mahakama kuwa hajamuoa Bi. Ngoma kwa sababu hana fedha za kufanya hivyo. Aidha, ameongeza kuwa hakuwa anawasiliana na binti huyo kwa madai kuwa alikuwa anampuuzia.

Kwa mujibu wa gazeti hilo, Hakimu Evelyne Nalwiyze aliyekua anasikiliza kesi hiyo ameamshauri Bi. Ngoma kumshitaki mwanaume huyo kwa kuvunja makubaliano ya ndoa.

Hakimu amesema kuwa mahakama haiwezi kuendelea na kesi hiyo kupata usuluhishi kwa sababu hakuna ndoa kati yao licha ya kuwa mahari imelipwa.

Gazeti hilo limeeleza kuwa Hakimu Nalwihze alisema kuwa usuluhishi unatafutwa kwa wanandoa.

Send this to a friend