![](https://swahilitimes.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/gr-og_image-1-814x613.webp)
Familia moja katika Kijiji cha Kirima, eneo la Ngaru, Kaunti ya Kirinyaga nchini Kenya imepatwa na mshtuko mkubwa baada ya binti yao mwenye umri wa miaka 26 kuuawa kikatili, baada ya kumtembelea mpenzi wake jijini Nairobi.
Kwa mujibu wa baba wa binti huyo, James Munene amesema mwili wa Lisper Ng’endo ulipatikana Kajiado, siku nne baada ya kuondoka nyumbani kuelekea Nairobi, na kwamba mtuhumiwa anadaiwa alikiri kwa dada wa mke wake kwamba alimuua Lisper na kutupa mwili wake ukiwa na majeraha huko Kajiado, kisha kutoweka.
Dada wa marehemu, Caroline Wandia, amesema kuwa Februari 1, 2025, Lisper aliondoka kituo cha mabasi cha Kerugoya saa kumi jioni baada ya kupokea simu kutoka kwa mwanaume huyo, ambapo waliwasiliana hadi alipofika kwa mpenzi wake na kisha hakupatikana tena hewani.
Familia ya binti huyo imeeleza kuwa inashindwa kuelewa kwa nini Lisper ameuawa na mtu ambaye alikuwa naye katika uhusiano kwa zaidi ya miaka sita.
“Alikuwa ametembelea nyumbani kwetu Kirima mara kadhaa, na dada yangu alikuwa hata ametembelea familia yake huko Kericho. Tulikuwa tukisubiri ndoa yao,” ameeleza Wandia.
Familia pia imeeleza kuwa mwanaume huyo alidai kuwa ni Afisa mkuu wa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) huko Nairobi, lakini baadaye waligundua kuwa alikuwa anafanya kazi kama mlinzi wa shamba huko Kajiado.
Aidha, familia hiyo imeomba vyombo vya usalama kumkamata kijana huyo na kufunguliwa mashitaka.