
Jeshi la Polisi mkoani Tabora linamshikilia Christina Nashoni (15), mkazi wa Kijiji cha Malagarasi, Wilaya ya Kasulu, mkoani Kigoma, kwa tuhuma za kujaribu kutorosha mtoto mchanga wa kike mwenye umri wa miezi mitatu kutoka kwa mwajiri wake, Beatrice Kiboma, mkazi wa Cheyo B, Manispaa ya Tabora.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Richard Abwao, tukio hilo lilitokea Machi 19, 2025 ambapo inadaiwa kuwa Christina alitoka nje ya nyumba akidai anaenda kuanika nguo, lakini badala yake alitoka nje ya geti na kujaribu kutoroka na mtoto huyo.
Taarifa ya awali ya polisi imesema kuwa Christina alitaka kumtorosha mtoto huyo ili kumpeleka kwao Kasulu, kwa sababu alipokuwa anaondoka kijijini kwao alidanganya kuwa ni mjamzito.
Ameeleza kuwa mnamo Machi 19, 2025, majira ya saa tisa na robo alasiri, katika eneo la kituo cha mafuta, Kata ya Kanyeye, mtuhumiwa alikamatwa na wananchi wakishirikiana na polisi akiwa anatoroka na mtoto Daniel Dotto, mwenye umri wa miezi mitatu na wiki moja.
Hata hivyo, polisi wamesema binti huyo alifanya kazi kwa siku moja tu, kisha aliamua kuondoka kwa madai kuwa kazi ni nyingi, na ndipo alipoamua kutoroka na mtoto wa mwajiri wake.
Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi ili kubaini kama kuna sababu nyingine zilizosababisha binti huyo kufanya tukio hilo.