Dar es Salaam, Tanzania
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dotto Biteko, ameeleza kuwa Watanzania wamekuwa wakisikitishwa na mzunguko wa bei za mafuta ambazo mara nyingine hupanda wakati huo huo na kisha kushuka haraka. Serikali imetangaza mipango ya kupitia upya bei za mafuta ili kuhakikisha Watanzania wanapata bei halisi na nafuu.
Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri Biteko alisema kuwa ingawa kuna sababu za kimataifa zinazosababisha gharama ya mafuta kupanda, kuna sababu nyingine zinazohitaji kushughulikiwa ili kuleta unafuu nchini.
“Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kwenye upangaji wa bei, hili ni jambo ambalo linawapa simanzi sana Watanzania kwamba kila wakati bei inapotaka kubadilika, kipindi hicho hicho utaona mwishoni pale mafuta yanaadimika, na baada ya muda bei ikitokea mpya utaona hali inarudi kawaida. Sasa huo ni mchezo ambao Watanzania hawawezi kufanyiwa kwa muda wote,” alisema.
Nchi 10 za Afrika zenye bei ya juu zaidi ya mafuta kwa Septemba
Waziri Biteko aliongeza kuwa ni muhimu kwa wafanyabiashara wa mafuta kutambua wajibu wao wa kuhudumia Watanzania na si kuzingatia faida pekee.
“Hii kazi si ya Serikali peke yetu, tunawaomba wafanyabiashara na wao wajue wanawajibu wa kuwahudumia Watanzania kwa leseni walizopewa wafanye kwa uaminifu. Hakuna mafuta tunajua, volume ya uagizaji wa mafuta imepungua lakini Serikali inachukua hatua za haraka kuhakikisha hiyo gepu inaifunika,” alisema.
Alitoa hakikisho kwa Watanzania kwamba Serikali imejipanga kuchukua hatua za kudhibiti changamoto za bei za mafuta nchini.