Biteko: Upungufu wa umeme umepungua baada ya mvua kunyesha

0
37

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa kishirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) linafanya kila liwezekanalo kuhakikisha tatizo la upungufu wa umeme nchini linatatuliwa.

Akizungumza bungeni Dodoma leo amesema uzembe ndani ya TANESCO hauwezi kuvumiliwa hivyo ikiwa kuna mtu anakwamisha juhudi za Serikali za kuhakikisha tatizo hilo linatatuliwa atachukuliwa hatua haraka iwezekanavyo.

“Inawezekana tusitangaze tumechukua hatua gani, tunachukua hatua za ndani kila inapoitwa leo, mtu yeyote ambaye anatukwamisha mahali fulani tunahakikisha yeye anakwama kwanza kabla ya wananchi kukwama. Wananchi wanataka umeme,” amesema.

Amesema upungufu wa umeme nchini umeendelea kupungua kutokana na ongezeko la mvua zinazoendelea kunyesha katika mabwawa ya uzalishaji, akitolea mfano Bwawa la Mtera ambalo ilishuka kiwango cha maji na kufikia mita 689 na kwa sasa imefikia mita 695 ikiwa bado mita tatu kufikia kwenye kiwango cha juu cha uzalishaji wa umeme.

“Mwezi wa tisa tulikuwa na upungufu uliokuwa unaelekea megawati 400, ninafurahi kusema kwamba baada ya mvua kunyesha, ukarabati wa mitambo, kuongeza gesi kwa maana ya mkandamizo wa gesi, upungufu huo umeendelea kupungua. Hivi ninavyozungumza tuna upungufu wa megawati 193 kwenye gridi ya taifa,” ameeleza.

Send this to a friend