Bobi Wine asema katiba mpya pekee si suluhisho

0
39

Wakati hoja ya Katiba Mpya ikitawala mijadala na hotuba za viongozi mbalimbali katika Baraza Kuu la CHADEMA, mwanasiasa wa upinzani kutoka nchini Uganda ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye baraza hilo amesema katiba mpya pekee haiwezi kuwa mwarobaini wa matatizo.

Robert Kyagulanyi maarufu Bobi Wine ambaye ni kiongozi wa chama cha National Unity Platform amesema ni wazo zuri kuwa na katiba mpya, lakini isichukuliwe kama ndio itamaliza matatizo yote kwenye nchi husika.

“Uganda tuna katiba nzuri sana, naweza kusema moja ya katiba bora zaidi duniani licha ya kuwa Jenerali [Rais Yoweri] Museveni amebadili katiba mara nyingi sana. Katiba yetu haiheshimiwi, sheria nchini Uganda ni nzuri tu kama ilivyo kwenye karatasi ilimoandikwa,” ameeleza.

Akitoa mbadala wa hayo amesema kuwa ni lazima kuwajengea uwezo wananchi waweze kuisimamia katiba ambayo wanakusudia kuwa nayo.

Ametoa wito kwa CHADEMA kuwashawishi vijana zaidi kushiriki kwenye shughuli za kisiasa kwani Afrika ni bara changa, na hivyo hatma ya Afrika ipo mikononi mwao, kwa wao kujua ni wapi wanakusudia kwenda.

Send this to a friend