Bodaboda Tanga wachoma basi la Saibaba lililomgonga mwenzao

0
62

Basi la Kampuni ya Saibaba Express lililokuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea mkoani Arusha limechomwa moto na kundi la bodaboda katika Kata ya Mtonga, Halmashauri ya wilaya ya Korogwe mkoani Tanga baada ya mwenzao kugongwa na basi hilo wakati likijaribu kupita lori eneo lisiloruhusiwa.

Akizungumza na Swahili Times Kamishina Msaidizi wa Polisi mkoani humo, Almachius Mchunguzi amesema ajali hiyo imetokea Februari 27, 2024 majira ya saa saba mchana ambapo baada ya bodaboda kupata taarifa ya mwenzao kugongwa waliamua kulifuatilia basi hilo na kulichoma moto.

“Hakuna abiria aliyejeruhiwa, kwa bahati nzuri abiria waliweza kutoka salama na kutoa baadhi ya vitu vyao, lakini vitu vichache tu ndio vimeungua, lakini asilimia kubwa ya vitu vingi abiria walitoa,” ameeleza Kamishna.

Ameongeza kuwa bodaboda aliyegongwa na basi hilo amefariki mara baada ya kufikishwa hospitali kwa ajili ya matibabu.

Aidha, amesema mpaka sasa jeshi la polisi linamshikilia dereva wa basi hilo kwa ajili ya mahojiano zaidi, huku likiendelea na uchunguzi kwa yeyote aliyehusika kufanya uhalifu wowote ili sheria ichukue mkondo wake.

Send this to a friend