
Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari imeelekeza waandishi wa habari waliotangaza nia ya kugombea nafasi za kisiasa kusitisha mara moja shughuli zote za kihabari katika kipindi chote cha mchakato wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na bodi hiyo imesema hatua hiyo inalenga kuepusha mgongano wa kimaslahi, kulinda uaminifu wa vyombo vya habari na kuweka mazingira ya usawa kwa wagombea wote, na kwamba kuendelea kushiriki shughuli za kihabari ni ukiukaji wa kanuni ya 12(g) ya Kanuni za Utangazaji wa Uchaguzi kwa Vyama vya Siasa.
Aidha, bodi hiyo imewataka waandishi wote wanaofanya kazi katika vyombo vyote vya habari vya kielektroniki au vya machapisho bila kusajiliwa na bodi hiyo kuacha mara moja kufanya kazi hizo hadi watakapokamilisha usajili kupitia mfumo wa TAI HABARI.
“Kuendelea kufanya kazi pasipo kusajiliwa na bodi ni ukiukaji wa kifungu cha 19 cha Sheria ya Huduma za Habari, Sura ya 229 (Toleo la 2023) ambacho kinakataza mtu yeyote kufanya kazi za kihabari bila kupewa ithibati,” imeeleza taarifa.
Bodi hiyo imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia kwa ukaribu mwenendo wa waandishi wa Habari wote nchini, na kwamba haitasita kuchukua hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwataja hadharani watakaobainika kukiuka masharti ya Sheria, Kanuni na Maadili ya taaluma ya uandishi wa habari.







