Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imewataka wadau wote wa mpira wa miguu walioteuliwa kuwania Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF) kwa mwaka 2023 kuhakikisha wanahudhuria bila kukosa sherehe za tuzo za ligi kuu zilizopangwa kufanyika Juni 12, mwaka huu jijini Tanga.
Katika taarifa yake TPLB imesema wateuliwa wa tuzo hizo wanalazimika kuhudhuria tukio hilo kwa mujibu wa kanuni ya 11:9 ya ligi kuu kuhusu vikombe na tuzo, na kwamba endapo utaratibu huo utakiukwa hatua za kinidhamu zitachukuliwa.
“Mteule yeyote atakayeshindwa kufuata utaratibu, maelekezo na kushindwa kuhudhuria sherehe za tuzo bila ridhaa ya TFF/TPLB atachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo faini, kufungiwa michezo au kipindi fulani pamoja na kupoteza nafasi ya kuwa mshindi, na nafasi yake kuchukuliwa na mshindani anayemfuatia kutokana na vigezo,” imesema TPLB.