Bodi ya Mikopo yataja sababu kuu tatu za wanafunzi kukosa mikopo

0
75

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema kuwa wanafunzi wengi hususani wanaotoka katika kaya maskini wamejikuta wakikosa mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Serikali kutokana na kukiuka maelekezo yanayotolewa katika mwongozo wakati wa kujaza fomu za maombi mtandaoni.

Hayo yameelezwa na Meneja Mikopo wa HESLB Kanda ya Ziwa, Usama Choka ambapo amesema pamoja na nia njema iliyowekwa na Serikali katika kuhakikisha kuwa wanafunzi wananufaika na mikopo hiyo, bado miongoni mwao wamejikuta wakikosa fursa hiyo kutokana na kufanya makosa mbalimbali wakati wa kujaza fomu za maombi.

‘’Wanafunzi wengi wanaotoka katika kaya maskini hususani waliopo katika mikoa ya pembezoni, wamekuwa wakishindwa kukamilisha baadhi ya maelekezo yanayotolewa wakati wa kujaza fomu za maombi ya mikopo ya elimu ya juu kupitia mtandao, hivyo HESLB tumeamua kuanzisha programu ya elimu ya mafunzo ya jinsi ya kujaza fomu hizo ili kuongeza wigo wa wanufaika wa mikopo hii,’’ amesema Choka

Aidha, Choka amezitaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na waombaji wengi kusahau kupiga mihuri fomu, uwekaji wa saini ya mwombaji pamoja na mdhamini pamoja na kuacha kudhibiti cheti cha kuzaliwa katika mamlaka za serikali ikiwemo Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufulisi (RITA), na hivyo kufanya maombi yao kutofanyiwa kazi wakati wa zoezi la upangaji wa mikopo.

Kwa upande wake, Afisa Mikopo wa HESLB, Jonathan Nkwabi amewataka wanafunzi wanaotuma maombi ya mikopo kwa mwaka 2020/2021 kujihadhari na kundi la matapeli ambao mara kadhaa wamekuwa wakiwadanganya kuwa ni mawakala waliotumwa na ofisi hiyo huku wakidai kiasi cha fedha kwa ajili ya kuwasaidia wakati wa kutuma maombi yao.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru bajeti ya TZS 464 bilioni kwa mwaka 2020/2021 imeongezeka kutoka TZS 450 bilioni mwaka 2019/2020 ambazo ziliwanufaisha jumla ya wanafunzi 132,119, ambapo ongezeko hilo la bajeti inatokana na adhma ya serikali ya kupanua wigo wa elimu ya juu hususani kwa wanafunzi wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo wa kiuchumi.

Send this to a friend