Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imetangaza kusimama kwa michezo ya Ligi Kuu ya NBC hadi Machi 1, 2025 itakaporejea kwa michezo ya mzunguko wa 17.
TPLB imesema chanzo cha kusimama kwa ligi ni kupisha michuano ya kuwania Kombe la Mapinduzi itakayofanyika Kisiwani Pemba pamoja na Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani (CHAN) ambapo Tanzania ni moja ya wenyeji.
“Bodi ya Ligi Kuu inaamini klabu zake zitatumia kipindi hiki kufanya marekebisho na maboresho katika vikosi vyake ili kuendana na ushindani mkubwa uliopo kwenye Ligi Kuu ya NBC msimu huu,” imesema taarifa.
Aidha, Bodi hiyo imesema imejipanga kuhakikisha msimu wa 2024/2025 unafikia tamati kwa wakati kwa mujibu wa kanuni za ligi na kutoathiri kipindi cha mapumziko na maandalizi ya msimu wa 2025/2026.