Bondia Mayweather atumika katika kampeni za uchaguzi Zimbabwe

0
38

Bingwa wa zamani wa ndondi duniani, Floyd Mayweather amehudhuria mkutano wa kampeni ya kisiasa nchini Zimbabwe siku ya Alhamisi, ikiwa ni sehemu ya kuwashawishi wapigakura hususani vijana kumchagua Rais Emmerson Mnangagwa (80) kuwa Rais wa nchi hiyo kwa awamu ya pili.

Mayweather (46) ambaye ni raia wa nchini Marekani, amekaribishwa kwa nyimbo na ngoma zilizopigwa na wafuasi wa chama cha ZANU PF huko Mabvuku, huku akisisimua umati kwa mazoezi yake ambayo ni pamoja na ngumi na kuruka kamba, na kupata nafasi ya kutazama mechi tatu kutoka kwa mabondia chipukizi wa Zimbabwe.

Mmoja wa washirika wa karibu wa Rais Emmerson Mnangagwa, Scott Sakupwanya anayetazamia kugombea kiti cha ubunge kutoka jimbo linalomilikiwa na upinzani, ameviambia vyombo vya habari kuwa ndiye aliyemwalika Mayweather kwenye mkutano huo.

Kenya: Jaji Mkuu Mstaafu apigwa mabomu akitaka waandamanaji waachiwe

“Watu walidhani nilidanganya niliposema nitamleta Mayweather, lakini yuko hapa. Hii inaonesha kwamba kile nitakachoahidi katika uchaguzi huu kitatimia,” amesema Sakupwanya.

Hata hivyo, baadhi ya vijana waliohudhuria mkutano huo wameahidi kumpigia kura Mnangagwa katika uchaguzi wa Agosti 23 akichuana na chama cha Citizens Coalition for Change (CCC) huku taifa hilo likikumbwa na mzozo wa kiuchumi na mfumuko wa bei.

Send this to a friend