Bosi Tigo ‘akataa’ kuongeza mkataba

0
20

Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Tigo Tanzania, Simon Karikari anatarajia kuondoka kwenye kampuni hiyo kufuatia kuamua kutoongeza mkataba, pindi mkataba wake wa sasa utakapokwisha mwishoni mwa mwezi huu.

“Mkataba wake unakwisha mwishoni mwa mwezi huu. Alinitaarifu mapema kwamba hatoomba kuongeza,” amesema Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Tigo, Ami Mpungwe.

Karikari anaondoka Tigo baada ya kuitumikia kwa miaka saba, ikiwemo mitano hapa nchini. Alianza kuitumikia Tigo Aprili 2016 akiongoza idara ya fedha (Chief Financial Officer), nafasi aliyoshika hadi Mei 2017 alipoteuliwa kuwa CEO.

Wakati akichukua majukumu hayo mapya Tigo ilikuwa na takribani wateja milioni 11.37, na anaondoka ikiwa na wateja milioni 13.01. Aidha, wateja wa Tigo Pesa wameongezaka kufikia milioni 8.4 kutoka milioni 6.05 katika kipindi hicho.

Kuondoka kwa Karikari kunakuja miezi michache baada ya kampuni ya Milcom kutangaza inaiuza Tigo na Zantel kwa kampuni ya Axian Group ya Madagascar.

Send this to a friend