Bosi wa uwanja wa ndege Kenya atimuliwa baada ya umeme kukatika

0
45

Waziri wa Uchukuzi nchini Kenya, Kipchumba Murkomen amefuta mkataba wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya (KAA), Alex Gitari na Meneja Mkuu wa Uhandisi, Fred Odawo kufuatia kukatika kwa umeme na kusababisha abiria katika Uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi kuhangaika gizani.

Waziri Murkomen ameomba radhi kufuatia tukio hilo lilitokea siku ya Ijumaa usiku na kusababisha usumbumbufu mkubwa kwa wasafiri.

Video zilizorushwa mtandaoni kutoka kituo cha utangazaji cha NTV zilionyesha wasafiri wakiwa wamejibanza gizani katika eneo la uwanja huo, huku wengine wakitumia tochi za simu kupata mwanga.

“Napenda kuomba radhi kwa wasafiri na watumiaji wa uwanja wa ndege ambao walikuwa wameathiriwa kwa njia moja au nyingine na kukatika kwa umeme katika JKIA,” amesema Murkomen.

Aidha, amesema tayari wizara imeanza mchakato wa kuajiri wafanyakazi wapya kuchukua nafasi hizo katika zoezi litakalokamilika ndani ya wiki mbili zijazo.

“Nawahakikishia nchi na dunia nzima kwamba tumechukua hatua za kuimarisha uwezo wa wataalamu wa kiufundi katika idara ya uhandisi ili kuhakikisha kwamba tukio kama hili halijirudii,” ameeleza.

Send this to a friend