Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema hakuna mtu au kampuni yoyote inayoruhusiwa kuikataa shilingi ya Tanzania kwa malipo yoyote halali, kwani ndiyo fedha pekee ambayo inaruhusiwa kutumika nchini.
Katika taarifa yake imesema Serikali ilishatoa tamko kuhusu katazo la matumizi ya fedha za kigeni kwa wakazi wa Tanzania katika kulipia bidhaa na huduma nchini, na kwamba kitendo cha kukataa malipo kwa shilingi ya Tanzania ni kuvunja sheria ya Benki Kuu ya Tanzania ya mwaka 2006.
Rais Samia: Mashirika yanayoitia hasara Serikali tutayafuta
“Benki Kuu inapenda kuukumbusha umma kwamba maagizo yaliyotolewa hapo awali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni yanapaswa kuendelea kuzingatiwa kuwa bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania, bei hizi zinajumuisha kodi za kupangisha ardhi, nyumba na ofisi, gharama za elimu, huduma za afya, vifaa tiba na vitendanishi, gharama za usafiri, lojistiki za bandari, vifaa vya kielektroniki na huduma za mitandao ya mawasiliano,” imesema taarifa ya BoT.
Aidha, BoT imesema bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni, na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni ambazo ni pamoja na gharama za hoteli, usafiri, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania na gharama za mizigo bandarini.