
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), noti ya Shilingi 10,000 ndiyo noti inayotumika zaidi nchini Tanzania, ikichangia zaidi ya asilimia 85 ya fedha zote zinazozunguka nje ya mfumo wa benki.
Kwa mujibu wa BoT, zaidi ya Shilingi trilioni 7.1 katika noti za TZS 10,000 zipo kwenye mzunguko kwa ajili ya matumizi ya kila siku kote nchini. Ikilinganishwa na hilo, noti za Shilingi 5,000 zinawakilisha Shilingi bilioni 674, noti za Shilingi 2,000 zikiwa Shilingi bilioni 279, noti za Shilingi 1,000 zikiwa Shilingi bilioni 199, na noti za Shilingi 500 zikiwa Shilingi bilioni 60 pekee.
Sarafu zinatumiwa kwa kiwango kidogo zaidi, ambapo sarafu za Shilingi 200 zikiwa na thamani ya Shilingi bilioni 50, Shilingi 100 zikiwa Shilingi bilioni 34, na sarafu za Shilingi 50 zikiwa Shilingi bilioni 16.
Aidha, Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba, ameeleza kuwa baada ya msimu wa mavuno, hasa kati ya Agosti na Septemba, wakulima hupokea kiasi kikubwa cha fedha wanapouza mazao kama vile mahindi na mpunga, na katika hali kama hizo, noti ya Sh10,000 hupendelewa kwa urahisi wa kubeba na kutumia.
Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaeleza kuwa utawala wa noti hiyo unatokana pia na hali ya uchumi wa Tanzania unaotegemea zaidi miamala ya fedha taslimu, tofauti na nchi zilizoendelea zinazotumia zaidi mifumo ya malipo ya kidijitali.