BoT: Unaporudishiwa fedha chakavu usikatae

0
91

Kufuatia kuwepo kwa mivutano katika huduma mbalimbali za umma pindi mwananchi anaporudishiwa pesa iliyo chakavu, Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imeshauri wananchi kutokataa pesa hizo ikiwa ni halali badala yake itumike utaratibu wa kuzipeleka benki ili ziweze kubadilishwa.

Akizungumza na Swahili Times, Meneja Msaidizi Kitengo cha Mawasiliano, Noves Moses amesema jukumu la Benki Kuu ni kusimamia mabenki (commercial banks) hivyo zinapaswa kuzipokea na wao hufanya mchakato wa kuziharibu na kurudisha pesa mpya.

“Inapokufikia noti ambayo unaona ni chakavu, basi tumia utaratibu uliopo kuipeleka kule inakohusika ili iweze kuchukuliwa na kwenda kufanyiwa utaratibu unaouhusika kufanyiwa kwa maana ya kuwa destroyed [kuharibiwa] ili tuweze kupata noti mpya kwenye mzunguko wetu,” amesema.

Adha, amesema pesa inaweza kukataliwa benki kutokana na kutokuwepo kwa alama mbalimbali muhimu ambazo zinaainisha uhalali wa noti, hivyo wananchi wanapaswa kutambua alama hizo kabla hawajapeleka katika mahali husika kwa ajili ya kubadilishwa.

Mkuu wa Wilaya ashitakiwa kwa kutusi na kuwaweka mahabusu watumishi

Amesema pia kuwepo kwa pesa nyingi chakavu ni kutokana na wananchi kutokuwa na elimu ya utunzaji wa pesa na kutotilia umakini wa umuhimu wa kutunza noti.

Ameongeza kuwa Serikali inatumia gharama kubwa kutengeneza pesa hizo, hivyo ni vyema wananchi watambue umuhimu wa kutunza noti na sarafu vizuri ikiwemo kuepuka kuzikunjakunja wanapozihifadhi ili ziweze kudumu kwa muda mrefu.

Send this to a friend