BoT: Wakopeshaji wa mtandaoni tunaowatambua ni wanne pekee

0
45

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema kati ya maombi 16 ya ‘aplikesheni’ yaliyopokelewa kwa ajili ya kutoa mikopo mitandaoni, manne pekee ndiyo yamekidhi vigezo na kupewa leseni za kukopesha mtandaoni huku aplikesheni 55 zilikabidhiwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ziondolewe mtandaoni.

AKizungumza na gazeti la Nipashe, Meneja Msaidizi Idara ya Huduma Ndogo za Fedha BoT, Mary Ngasa amesema programu zilizopewa kibali zinatakiwa kuweka wazi kuwa zinafanya kazi kwa mujibu wa leseni inayotolewa na BoT, kuweka wazi masharti ya mikopo pamoja na mawasiliano ambayo wateja wanaweza kuwasiliana nao kwa jambo lolote.

Aidha, amesema BoT imebaini ukiukwaji wa sheria kwa watoa huduma ndogo za fedha (microfinance) kwa kuanzisha programu za kukopesha mtandaoni kinyume cha sheria zilizowekwa.

“BoT imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya microfinance nne ambazo zilianzisha aplikesheni na kutoa mikopo mtandaoni bila kibali cha BoT kama leseni yao inavyowataka,” amesema.

Ameongeza, “Wanaotoa mikopo mtandaoni bila kibali, waliogundulika hadi sasa ni 55, na licha ya tangazo kuwataka wajisajili hawajafanya hivyo. Tulivyotoa mwongozo wa kuwataka walete maombi hawajaleta, lakini tumewafuatilia mtandaoni na kuwabaini.”

Send this to a friend