
Rais wa Botswana, Duma Boko ametangaza hali ya dharura ya afya ya umma baada ya nchi hiyo kukabiliwa na uhaba wa dawa muhimu na vifaa vya matibabu kutokana na hali ya uchumi.
Wizara ya Afya imesema kuna uhaba wa dawa kwa magonjwa kama shinikizo la damu, kisukari, kifua kikuu, pumu, kansa, matatizo ya akili, magonjwa ya ngono, sindano na vifaa vya kufunga majeraha.
Rais Boko amesema jeshi litasimamia usambazaji wa dawa haraka, na kipaumbele kipo kwa wakazi wa vijijini huku akieleza kuwa bei za dawa sasa zinaweza kupanda mara 5 hadi 10 kutokana na uchumi mgumu.
Tatizo hilo limehusishwa na kupungua kwa mapato ya almasi, ambayo ni chanzo kikuu cha mapato ya nchi pamoja na kupungua kwa misaada ya Marekani kutokana na sera ya Donald Trump.








