Bunge la 12 halitokuwa na Kambi Rasmi ya Upinzani

0
43

Wakati vikao vya Bunge la 12 la Tanzania vikianza leo jijini Dodoma, bunge hilo litakuwa na muundo tofauti kidogo na Bunge la 11, ambapo katika bunge la sasa hakutakuwa na Kambi Rasmi ya Upinzani.

Hayo yamesema na mgombea wa nafasi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai wakati akinadi sera zake mbele ya wabunge na kuwaomba kumchagua ashike nafasi hiyo kwa kipindi cha pili.

“… hatutakuwa na Kambi Rasmi ya Upinzani kwa kuwa hawataweza kutimiza asilimia 12.5 ambayo ipo katika kanuni yetu,” amesema Ndugai.

Akijibu swali la Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Aida Khenani (CHADEMA), Ndugai amesema licha ya kambi hiyo kutokuwepo, wabunge wa CCM ambao wengi ni vijana kwa kushirikiana na ofisi ya spika, watawatendea haki wabunge wa upinzani.

Vyama vya upinzani vilipata jumla ya wabunge nane (CHADEMA 1, ACT Wazalendo 4 na CUF 3) katika uchaguzi mkuu uliofanyoka Oktoba 28 mwaka huu. Pia, kutokana na idadi kubwa ya kura za wabunge, CHADEMA imepata nafasi ya kuteua wabunge 19 wa viti maalum, hata hivyo chama hicho hakijafanya uteuzi huo.

Endapo CHADEMA itateua wabunge hao, jumla ya wabunge wa upinzani bungeni watakuwa 27, lakini sisipowateua, wabunge wa upinzani watakuwa nane, idadi ambayo ni ndogo sana ikilinganishwa na bunge lililopita.

Katika mkutano wa kwanza wa bunge uliaoanza leo mambo kadhaa yanatarajiwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kuthibitisha uteuzi wa waziri mkuu, kuchagua spika na naibu spika, kiapo cha uaminifu kwa wabunge na kusomwa kwa tangazo la Rais la kufungua bunge.

Send this to a friend