Bunge la Tanzania leo limepitisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Huduma za Habari sura ya 229 ambapo kifungu cha 5 kilipendekezwa kufanyiwa marekebisho kwa lengo la kumuondolewa Mkurugenzi Idara ya Huduma za Habari jukumu la uratibu wa matangazo yote ya Serikali.
Pia, maboresho hayo yamefanyika kuiwezesha Serikali kuwa na uhuru wa kuchagua chombo cha habari itakachokitumia kwa ajili ya matangazo kwa kuzingatia nguvu ya ushindani katika soko, pamoja na kukifanyia marekebisho kifungu cha 38 kwa madhumuni ya kuongeza haki ya uhuru wa maoni.
Sakata la kelele, Waziri Mkuu atoa maagizo kwa wakuu wa mikoa
Akiwasilisha Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali bungeni Dodoma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Dkt. Eliezer Feleshi amependekeza marekebisho kwenye vifungu vya 50, 51, 53, 54, 55, 63 na 64 kwa madhumuni ya kuweka adhabu tahafifu kwa makosa yatokanayo na ukiukwaji wa sheria ili kuwafanya wanahabari kujirudi na kufurahia kazi zao.
Aidha, Dkt. Feleshi amesema marekebisho ya vifungu hivyo yanakusudia kuondoa adhabu kwa wamiliki wa mitambo ya uchapishaji, ambao katika hali ya kawaida hawana uwezo wa kudhibiti maudhui yanayochapishwa katika mitambo hiyo ya uchapishaji.