Bunge lashauri wanaofariki wazikwe kwenye maeneo yao

0
43

Spika wa Bunge la Tanzania, John Ndugai ameshauri watu kuzikwa kwenye maeneo yao pindi wanapofariki, kwani kwa kutokufanya hivyo kunapelekea baadhi kuhofia kwenda hospitali.

Ndugai ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma wakati akielezea utaratibu wa sasa wa serikali ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakizikwa wanapofarikia, jambo ambalo baadhi ya wabunge wamesema linaleta simanzi kwa ndugu wa marehemu.

“Tatizo la jambo hili bila kuangaliwa vizuri, baadhi ya watu wengi sana hawatapelekwa hospitali kwa sababu wanafamilia watafikiria, tukimpeleka mpendwa wetu, kurudi ni maajaliwa, kwamba kapona. Lakini asipopona ndio basi,” amesema Ndugai.

Ndugai ameeleza kuwa ile fikra kwamba ndugu yao asipopona ndio kwaheri, wataona ni heri wabaki naye nyumbani, hata akiwafia angalau watapata nafasi ya kumzika.

Ameishauri serikali kuliangalia upya suala hili hata kama itakuwa ni kwa gharama za wafiwa kuhakikisha kuwa tahadhari zote zinachukuliwa, na aliyefariki anarudishwa kwao, kwani hilo litatoa moyo watu kwenda hospitali.

Spika ametolea mfano wa wabunge wawili waliozikwa hivi karibuni, Getrude Rwakatare na Richard Ndassa, ambapo tahadhari zote zilichukuliwa na wakazikwa kwenye maeneo yao jambo lililofariji familia.

Send this to a friend