Bunge la Tanzania limeishauri serikali kuvifanyia marejeo viwango vya fedha vya Mfuko wa jimbo ili viendane na hali ya sasa ya uchumi.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Daniel Baran Sillo wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji wa shughuli za kamati kwa mwaka mmoja uliopita.
Sillo amesema kuwa viwango vinavyotumika kutoa fedha kwa Mfuko wa Jimbo vilipangwa miaka karibia 20 iliyopita na havijawahi kurejewa mpaka hivi sasa.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati, thamani ya shilingi inaanguka kwa wastani wa asilimia 3 hadi 5 kila mwaka, hivyo kupunguza uwezo wa fedha kununua bidhaa na huduma.
Kamati imetoa mfano wa mfuko wa saruji miaka 20 iliyopita ulikuwa kati ya shilingi 10,000 hadi 15,00, hivi sasa ni shilingi 18,000 hadi 25,000 hivyo ni wazi kwamba uwezo wa kufanya manunuzi wa fedha za Mfuko wa jimbo umepungua kwa takribani asilimia 50.