Bunge latekeleza agizo la Rais Samia kuhusu bima ya afya

0
22

Bunge la Tanzania leo limepitisha muswada wa marekebisho ya Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ambayo yanalenga kuongeza umri wa mtegemezi kutoka miaka 18 hadi miaka 21.

Hatua hiyo imekuja ikiwa ni miezi minne tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipotoa maelekezo hayo wakati akizungumza kwenye Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) mkoani Mwanza.

“Serikali imeona mantiki ile iliyoletwa na Wafanyakazi kwamba mtoto wa miaka 18 bado ni mtegemezi kwa wazazi wake. Hivyo basi serikali tumeamua kuongeza umri wa utegemezi. Tutatoka miaka 18 hadi miaka 21,” alisema Rais Samia.

Sheria Namba 8 iliyoanzisha Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ya mwaka 1999 inawaondoka watoto kwenye utegemezi wakifikisha miaka 18, jambo ambalo limekuwa likikosolewa vikali kwamba sheria imekuwa ikiwaondoa wanafunzi kwenye utegemezi.

Katika hatua nyingine, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kuwa serikali inakusudia kupeleka bungeni muswada wa sheria utakaowezesha kuanzishwa kwa bima ya afya kwa wote, lengo likiwa ni kuimarisha huduma za afya na kuhakikisha kila mwananchi ana uhakika wa matibabu.

Mabadiliko hayo pia yanalenga kufikia lengo namba 3 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) ambalo linahimiza nchi zote duniani kuhakikisha ifikapo 2030, wananchi wake wanakuwa na afya bora kwa kuboresha huduma za afya katika ngazi zote kwenye jamii.

Send this to a friend