Katikati ya janga la corona Burundi imeendelea na kampeni za uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Mei 20 mwaka huu.
Taifa hilo ni miongoni mwa nchi ambazo zimeweka utaratibu kuwa mgeni au raia yeyote wa Burundi atakayeingia nchi humo atalazimika kukaa karantini kwa siku 14 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Mkakati huo utawaathiri pia waangalizi wa uchaguzi huo, kwani endapo watalazimika kukaa karantini siku 14, watakapotoa, uchaguzi utakuwa tayari umefanyika.
Kutokana na hilo, Burundi imeiandikia barua Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuisihi kutopeleka waangalizi badala yake itumie wataalam ambao wapo Burundi, huku ikiahidi kuwapa ushirikiano wa hali ya juu.
Katika uchaguzi huo raia wa Burundi watapiga kura kumchagua rais pamoja na wabunge. Endapo hakuna mgombea wa urais atakayepata kiwango cha kura kinachotakiwa (majority of the vote), uchaguzi mwingine utafanyika Juni 19 mwaka huu.