
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kukamilika kwa Mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Maji Kidunda kutaongeza uhakika wa upatikanaji wa huduma ya majisafi na Salama kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, na baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Morogoro.
Akizungumza na wakazi wa Kidunda Mkoani Morogoro mara baada ya kuweka jiwe la msingi kwenye Bwawa hilo linalojengwa na Serikali kwa gharama ya shilingi bilioni 335, Waziri Mkuu amesema bwawa hilo litaleta manufaa mengi, ikiwemo upatikanaji wa maji safi na salama, uzalishaji wa umeme, kuendeleza shughuli za uvuvi, na kuimarisha barabara ya Kidunda kutoka Ngerengere.
Aidha, ameeleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameelekeza kuwa mradi huo uliofikia asilimia 28 ni lazima uwanufaishe majirani wote wanaozunguka mradi huo, ikiwemo Tarafa nzima ya Ngerengere na vijiji vyake.
Kwa upande wake Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesisitiza kuwa wananchi ambao hawajalipwa fidia kutokana na utekelezaji wa mradi huo watalipwa stahiki zao na kuhakikisha kuwa haki za wananchi zinazohusiana na mradi huu zinazingatiwa.
Mradi wa Bwawa la Maji Kidunda unatarajiwa kuboresha maisha ya wakazi wa maeneo husika kwa kutoa maji ya uhakika, nishati ya umeme, na fursa nyingine za kiuchumi.