CAG: Mashine 89 za trafiki hazikuwahi kurekodi muamala wowote mwaka mzima

0
54

Utata umeibuka baada ya Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2020/21 kubaini kuwa mashine 89 ambazo zimetumiwa na Askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani kutoza faini kwa madereva wanaokiuka sheria, hazikuwahi kurekodi muamala wowote.

Hapa chini ni taarifa kama ilivyoandikwa kwenye ripoti ya CAG (UKAGUZI WA MIFUMO YA TEHAMA KWA MWAKA WA FEDHA 2020/21)

Usimamizi Duni wa Vifaa vya POS

Mfumo wa TMS hutumia vifaa vya ‘Point of Sale’ (POS) katika ukusanyaji wa ada na adhabu za makosa yatokanayo na ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani.

Vifaa vya POS husanidiwa inapotokea uhitaji, kwa hivyo POS zote zilizotolewa na kusanidiwa hazipaswi kukaa bila kutumika. Nilikagua mchakato wa kukusanya mapato ili kubaini ufanisi wa ubadilishanaji wa taarifa kati ya vifaa vya POS na mfumo wa TMS.

Ukaguzi wangu ulibaini kuwapo kwa POS 89 zilizosajiliwa na zilizopo hewani katika mfumo wa TMS ambazo hazijawahi kurekodi muamala hata mmoja kwenye mfumo. Uchambuzi wangu unaonesha kuwa vifaa vya POS vilivyobainishwa vilisajiliwa kati ya tarehe 1 Julai 2019 na tarehe 26 Februari 2021. Ufuatiliaji zaidi wa sampuli nne za vifaa vya POS mkoani Dodoma ulibaini kuwa vifaa hivyo havipo kwenye orodha ya rejista ya POS ya mkoa. Hii inamaanisha kuwa havitambuliki ijapokuwa vimesajiliwa kwenye mfumo.

Nilipoiuliza menejimenti ya Jeshi la Polisi Tanzania, ilinifahamisha kuwa POS 89 za ukusanyaji wa mapato ni mali ya Maxcom na, hivyo, si sehemu ya mfumo wa TMS. Menejimenti ilisisitiza kuwa POS hazitumiki. Hata hivyo, nilibaini kuwa vifaa hivi vya POS vilisajiliwa kati ya Julai 2019 na Februari 2021, kipindi ambacho mkataba kati ya TPF na Maxcom ulikuwa tayari umekwisha.

Ni maoni yangu kwamba hii imesababishwa na usimamizi duni wa vifaa vya POS ambayo inaleta mwanya wa vifaa kutumika katika kukusanya mapato nje ya mfumo wa TMS na GePG.

Napendekeza uongozi wa Jeshi la Polisi Tanzania kufuatilia vifaa vya POS vilivyobainishwa na kubaini sababu za kutokufanya miamala na kuhakikisha kuwa havitumiwi vibaya.

Send this to a friend