CAG: Deni la Taifa lafikia TZS trilioni 97.35

0
9

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles E. Kichere amesema kufikia Juni 30, 2024, deni la Serikali lilifikia shilingi trilioni 97.35 likiongezeka kutoka shilingi trilioni 82.25 katika mwaka wa Fedha 2022/2023, ikiwa ni ongezeko la shilingi trilioni 15.1 ambalo ni sawa na asilimia 18.36.

Akiwasilisha ripoti hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan Ikulu Dar es Salaam, Kichere amesema deni hilo linajumuisha deni la ndani la Shilingi trilioni 31.95 na deni la nje la shilingi trilioni 65.40.

Aidha, katika ripoti hiyo, Kichere ameeleza kuwa tathimini imebaini kuwa deni la taifa bado ni himilivu.

“Viashiria vikuu vinaonesha kuwa thamani halisi ya deni la nje ni asilimia 23.6 ya pato la taifa chini ya ukomo wa asilimia 40, na deni la jumla ni asilimia 41.1 ya pato la taifa chini ya ukomo wa asilimia 55,” amesema CAG.

Ameongeza kuwa malipo ya deni kwa mapato ya mauzo ya nje ni asilimia 127.5 chini ya ukomo wa asilimia 180, huku malipo ya deni kwa mapato ya Serikali ni asilimia 14.5 chini ya ukomo wa asilimia 18.