Canada: Uhusiano wa zamani na Marekani umekwisha

0
21

Waziri Mkuu wa Canada, Mark Carney amesema nchi hiyo italazimika kupunguza utegemezi wake kwa Marekani kwani uhusiano wao unazidi kuzorota.

Akizungumza baada ya mkutano wa baraza la mawaziri kuhusu vitisho vya ushuru kutoka kwa Rais Donald Trump, Carney amesema uhusiano wa zamani kati ya mataifa hayo umekwisha na Marekani si mshirika wa kuaminika tena.

“Uhusiano wa zamani tuliokuwa nao na Marekani, uliotegemea kuimarika kwa ushirikiano wa kiuchumi pamoja na usalama wa karibu na ushirikiano wa kijeshi, umekwisha,” amesema.

“Ni wazi kuwa Marekani si mshirika wa kuaminika tena. Inawezekana kwamba kupitia mazungumzo ya kina, tunaweza kurejesha kiwango fulani cha uaminifu, lakini hakutakuwa na kurudi nyuma,” amesema kiongozi huyo wa Canada, akiongeza kuwa serikali zijazo zitapaswa kukabiliana na mabadiliko hayo ya uhusiano.

Saa chache kabla ya Carney kuzungumza, Trump aliandika kwenye jukwaa lake la mtandao wa kijamii kwamba Canada na Umoja wa Ulaya zitakabiliwa na ushuru mkubwa, kuliko ilivyopangwa sasa, ikiwa watafanya kazi pamoja kuidhuru kiuchumi Marekani.