CCM kumuenzi Maalim Seif Sharif Hamad

0
41

 

Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Hayati Maalim Seif Sharif Hadama ataenziwa na Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa kuacha alama nzuri katika uongozi wake hasa wakati alipokuwa kijana na kiongozi mkubwa ndani ya chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa mfumo wa chama kimoja.

Amesema hayo leo akihutubia katika Kongamano la Kumbukizi ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad, mjini Unguja na kusisitiza kuwa nguli huyo wa siasa alikuwa daraja la amani na mtu aliyeongozwa na maono ya maslahi mapana ya taifa hivyo amani ya Zanzibar na Tanzania haiwezi kuzungumza bila kumtaja Maalim Seif.

“Tumemjua kama mtu wa kukutanisha watu, kiongozi wa watu, anayeishi na watu, aliyetokana na watu na watu wakamshiba katika mioyo yao. Huyo ndiye Maalim Seif Sharif Hamad,” ameeleza Rais.

Rais Samia amesema baadhi ya wanasiasa wanapotofautiana huanzisha vurugu zisizoisha tofauti na alivyokuwa Hayati Maalim Seif ambaye aliamini kumaliza tofauti zinazojitokeza kwa majadiliano na maridhiano, jambo ambalo Maalim Seif alisimamia wakati wote wa uhai wake.

Amesema jambo jengine ambalo Maalim Seif atabaki kukumbukwa ni tabia yake ya kupingana kwa kutumia hoja na sio lugha zisizo na staha kama ilivyo kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini.

Kongamano hilo la kwanza la kumbukizi ya maisha ya Maalim Seif limefanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Maalim Seif, Umoja na Maridhiano katika Ujenzi wa Zanzibar na Tanzania Mpya” .

Maalim Seif alifariki dunia Februari 17, 2021 akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam. Enzi za uhai wake alishika nafasi mbalimbali kwenye vyama vya siasa na serikali ambapo hadi anafariki alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Send this to a friend