CCM: Rais Magufuli ataja vigezo walivyotumia kuteua wagombea Ubunge na Uwakilishi

0
31

Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imekutana leo mjini Dodoma kwa lengo la kupitisha majina ya wanachama wa chama hicho walioteuliwa kugombea nafasi za Ubunge na Uwakilishi, visiwani Zanzibar.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao hicho, Mwenyekiti wa CCM, Rais Dkt. Magufuli amesema kuwa jumla ya wanachama 10,367 wa chama hicho waligombea nafasi za ubunge wa majimbo na viti maalum pamoja na uwakilishi, na kwamba wamepitia majina yote kwa kina.

“Uchambuzi wa majina ya wagombea ubunge na uwakilishi ulikuwa wa kina kweli kweli. Tulitumia taarifa nyingi ambazo tulizipata kutoka vyanzo mbalimbali, na mimi nataka kuwathibitishia wajumbe, nimesoma majina yote 10,367,” amesema Mwenyekiti wa CCM.

Akielezea uteuzi wa wagombea, amesema vikao vya awali vilivyokaa kabla ya kikao cha leo vimezingatia mambo mbalimbali katika uteuzi wa wagombea ikiwa ni pamoja na uongozi wa mgombea kuongoza na kujitoa kwake ndani ya chama.

“… vimejitahidi kuchambua na kupata wagombea wenye sifa zinazohitajika zikiwemo uwezo wa kuongoza, wazalendo, wenye kujitoa kwenye chama wanaofahamu mahitaji ya wananchi, wenye utayari wa kuwatumikia wananchi na Watazania wote na pia wenye kukubalika kwa wananchi,” amesema Rais Magufuli.

Kwa mujibu wa katika ya CCM, halmashauri kuu ya Taifa ya chama hicho ndiyo yenye mamlaka ya mwisho ya kuteua wagombea ubunge na uwakilishi.

Awali, Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally amesema kutokana na kutofautiana kwa ratiba za uchaguzi kati ya Tanzania Bara na Zanzibar, kikao cha leo kitapisha majina ya wagombea ubunge tu (majimbo na viti maalum).

Send this to a friend