CCM yaitaka Serikali kusikiliza maoni chanya ya wananchi kuhusu bandari

0
15

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimeielekeza Serikali kuhakikisha inasikiliza maoni chanya na yenye tija yanayotolewa na wananchi kuhusu makubaliano ya uwekezaji na uendelezaji wa bandari kati ya Tanzania na Dubai.

Wito huo umetolewa na Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) katika kikao chake cha kawaida chini ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan kilichofanyika Julai 09, jijini Dodoma.

Aidha, katika kikao hicho halmashauri imeazimia Serikali kuongeza kasi ya utoaji elimu kwa wananchi juu ya uhalisia uliomo katika makubaliano ya uwekezaji na uendeshaji wa bandari pamoja na kukubaliana kuwa uwekezaji na uendeshaji huo ni kwa manufaa ya uchumi wa nchi.

Katika hatua nyingine, taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya Habari na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) imewataka baadhi ya watu waliolalamika kutishiwa maisha yao na watu wanaodai wasiojulikana kutokana na kutoa maoni katika masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya taifa, kutoa taarifa Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika hao.

“Sambamba na hilo, kumekuwa na vitendo vya baadhi ya viongozi wa Serikali hususani mawaziri kutoa maonyo ambayo yanaashiria kuwatishia Watanzania wanaotekeleza uhuru wao wa kutoa maoni kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamii, vitendo vinavyoashiria kuanza kushuka kwa uhuru wa kujieleza hapa nchini,” imesema LHRC.

Mbali na hayo imetoa wito kwa Watanzania kutumia uhuru wao wa kujieleza kwa kuzingatia katiba na sheria za nchi bila kutweza utu wa mtu mwingine kwa vigezo vya jinsia, udini, ukabila, hadhi, ulemavu au rangi ya mtu.

Send this to a friend