CCM yaongoza kuweka wagombea nafasi zote wapinzani wakiwa na 38%

0
33

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mohamed Mchengerwa amesema Chama cha Mapinduzi (CCM), kimefanikiwa kuweka wagombea katika nafasi zote za vijiji, vitongoji na mitaa huku upinzani ukiweka wagombea 30,977 sawa na asilimia 38 ya nafasi zote 80,430 zinazoshindaniwa.

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akitoa tathmini ya uchaguzi wa serikali za mitaa, amesema nafasi zitakazogombewa kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 ni mwenyekiti wa kijiji nafasi 12,280, mwenyekiti wa mtaa nafasi 4,264 na mwenyekiti wa kitongoji nafasi 63,886, wajumbe wa serikali ya kijiji 230,834 na wajumbe wa kamati ya mtaa 21,320.

Amesema nafasi za mwenyekiti wa kijiji zinazogombewa ni 12,280 ambapo vyama 18 vya siasa viliweka wagombea katika nafasi 6,060 sawa na asilimia 49.35 ya nafasi hizo na nafasi za mwenyekiti wa mtaa zinazogombewa ni 4,264 ambapo vyama 18 vya siasa viliweweka wagombea katika nafasi 3,281 sawa na asilimia 76.94 ya nafasi hizo.

“Nafasi za mwenyekiti wa kitongoji zinazogombewa ni 63,886 ambapo vyama 18 vya siasa viliweka wagombea katika nafasi 21,636 sawa na asilimia 33.87 ya nafasi hizo,” amesema.

Amesema nafasi zote zinazogombewa ni 80,430 (ukitoa nafasi za wajumbe wa serikali za vijiji na kamati za mitaa), ambazo zinajumuisha vijiji 12,280, mitaa 4,264 na vitongoji nafasi 63,886.

Send this to a friend