CHADEMA: Hakukuwa na haja ya Serikali kuunda Kikosi Kazi

0
47

Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika amesema hakukuwa na haja ya Serikali kuunda Kikosi Kazi kwa sababu kazi ya kutafuta maoni ya wananchi ilifanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Oktoba 22, 2022 jijini Dar es Salaam ikiwa ni siku moja baada ya kikosi kazi cha kuratibu maoni ya wananchi kuhusu demokrasia ya vyama vingi, kukabidhi ripoti yake kwa Rais Samia Suluhu hapo jana, CHADEMA imeitaka Serikali kuweka wazi gharama ambazo kikosi kazi kimetumia.

Amesema maoni ya wananchi yalikusanywa na Tume ya Warioba, hivyo hakukuwa na haja ya kuundwa kwa kikosi kazi, bali wangerejea kwenye kitabu cha maoni ya wananchi kilichoandaliwa na Tume ya Warioba.

“Kuundwa kwa kikosi kazi ni matumizi mabaya ya fedha za Watanzania. Tunaitaka Serikali itoke hadharani ituambie kikosi kazi kimetumia fedha kiasi gani,” amesema.

Aidha, amedai kuwa walikuwa wakipigania kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara lakini baada ya kuundwa kwa kikosi kazi waliamua kukipa muda ili waone matokeo yake, lakini wameshangazwa na kauli ya Rais Samia wakati akijibu hoja hiyo akisema kuna haja ya kufanyia mabadiliko sheria na kanuni kabla mikutano haijaruhusiwa.

Send this to a friend