CHADEMA: Hatujawahi kujadili kuhusu serikali ya nusu mkate

0
47

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema hakijawahi kuletewa hoja ya kugawana madaraka kutoka Chama chochote au kutoka kwa Serikali wala hoja ya kupewa Majimbo ya Uchaguzi au kugawana nafasi za madaraka katika muundo wa Serikali.

Hayo yameelezwa katika taarifa ya ufafanuzi iliyotolewa kwa umma na chama hicho leo kufuatia kuibuka kwa hoja mbalimbali, ambapo chama hicho kimebainisha kuwa kwa mujibu wa Katiba iliyopo sasa, nafasi ya Makamu wa Rais hugombewa na haitolewi mezani, vilevile nafasi ya Waziri Mkuu hutokana na Chama chenye wabunge wengi Bungeni.

CHADEMA imesema kuwa katika vikao vyake vyote rasmi, haijawahi kujadili, kutoa au kupokea mapendekezo yeyote ya kitu kinachoitwa “Serikali ya nusu mkate” na kwamba jambo hilo halijawahi kuwa Sera ya Chadema.

“Chadema haijawahi kupokea wala kujadili au kubeba au kuwa na agenda na Serikali katika vikao vyote vya Chama au vile vya maridhiano kuhusu hoja hizo tajwa hapo juu”

“Ikumbukwe kuwa vikao vyote vya maridhiano vilifanyika mwaka 2022 na vikahitimishwa 3 Januari 2023 ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alizungumza na Taifa kupitia Vyama vya Siasa na wadau mbalimbali kuondoa katazo haramu la shughuli za kisiasa ikiwemo mikutano ya hadhara na maandamano.

Tarehe 30 na 31 May 2023 palifanyika vikao vya mwisho ambapo tulishindwana. Baada ya hapo hakuna kikao chochote cha siri au hadharani kimefanyika baina ya CCM na Chadema.” imeeleza taarifa.

Aidha, CHADEMA imewataka wanachama wake na viongozi wa chama hicho kuwekeza nguvu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji na kupuuza propaganda za kukigawa Chama.

Send this to a friend