CHADEMA Igunga wampongeza Rais Samia kwa kutatua changamoto zao

0
42

Wananchi wa Kata ya Mwisi Wilayani Igunga mkoani Tabora, wameipongeza Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia shule ya Sekondari ya Mwisi kiasi cha TZS milioni 642 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa nane, mabweni matatu na matundu 12 ya vyoo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti kijijini hapo, wananchi hao ambao ni wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wamempongeza Rais Samia kwa kuipatia fedha Kata hiyo za ujenzi wa madarasa na kwa kuendelea kutatua changamoto katika sekta ya Elimu, Afya na Maji, jambo ambalo limewapa matumaini makubwa na kuendelea kuiamini Serikali ya awamu ya Sita.

”Mimi ni Mwana-CHADEMA, katika miradi ya maendeleo ni lazima tuseme ukweli nikianzia katika elimu, siku za nyuma tulikuwa tunachangishwa fedha kila kaya lakini majengo yalikuwa hayaendi, lakini katika utawala wa Rais Samia madarasa, mabweni yanaota kama uyoga, leo nimetembelea hapa shuleni nimeona kazi zinapigwa, kwa kweli inatia moyo sana, ili kuwa na maendeleo bora inaitaji kuwa na viongozi bora,” amesema George Maige.

Huku Cosmas Kalwisa akiongeza kuwa ”Mimi pekee natanguliza shukrani zangu za dhati kwa mama yetu Rais Dkt Samia Suluhu Hassani kwa jitihada anazozifanya, nikizungumzia kata ya Mwisi kuna fedha zimetolewa kama milioni 642 na sasa hivi kazi inaendelea pale shuleni ya kujenga madarasa, mabweni na matundu ya vyoo yaani kazi inafanyika nzuri sana kiasi kwamba hata ukifika wakandarasi wanafanya kazi muda wote pia diwani Jambeck na walimu wanasimamia kazi muda wote.”

Kwa upande wake diwani wa kata hiyo, Ahamed Jambeck amempongeza Rais Samia kwa kuwaamini watendaji wake katika ngazi ya chini na kuendelea kuwapatia fedha nyingi za miradi ya maendeleo ikiwemo miradi ya afya, elimu, maji na umeme.

Send this to a friend