CHADEMA: Tutaitoa CCM madarakani mwaka 2025

0
53

Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mnyika amesema chama hicho kitahakikisha kinaimarisha majimbo yote ya Tanzania na Zanzibar ili kufikia dhamira ya kuiondoa CCM madarakani katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Ameeleza hayo wakati akihutubia katika mkutano mkuu wa jimbo la Geita Vijijini mkoani Geita akieleza kuwa “Tuna dhamira ya kushika dola mwaka 2025, kutokana na dhamira hii kuu, hatuwezi kuliacha jimbo lolote nyuma lazima yote tusonge kwa nguvu kamili. Ujumbe huu sio kwa Geita au kanda ya Victoria bali kanda zote 10 za Tanzania na Zanzibar.”

Aidha, amedai CHADEMA ndio chama cha tumaini kuu la Watanzania, akisema kama kunahitijaka mabadiliko ya uongozi, demokrasia na maendeleo, uhuru, haki za watu lazima kazi ya kujiimarisha ifanyike mahali kote ili chama hicho kiibuke kidedea na kuongoza Serikali mwaka 2025.

“Nyie wa Bukombe na Geita, kama ambavyo sisi wa kitaifa tutakavyozunguka katika majimbo na kata zote, nanyinyi mna wajibu wa kwenda kila kata, kijiji na kitongoji msiache mahali Chadema iamke ili kuwakomboa Watanzania,” amesema Mnyika.

Katika hatua nyingine, Mnyika amewataka wanachama wa chama hicho, kuutumia mwaka 2023 kudai Katiba Mpya na Tume huru ya uchaguzi akidai ni jambo linalopaswa kuwa la Taifa.

Send this to a friend