CHADEMA waruhusiwa kuandamana Mwanza, waonywa kutoikejeli Serikali

0
56

Jeshi la Polisi mkoani Mwanza limesema maandamano ya amani yaliyoandaliwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kupangwa kufanyika Februari 15 mwaka huu jijini humo, hayatazuiliwa endapo hayatasababisha uvunjifu wa amani, sheria za nchi au vitenodo vya kiuhalifu.

Katika taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Apolinary Ndibaika ameeleza kuwa viongozi wanachama na wafuasi wa CHADEMA wanalo jukumu la kuzuia lugha za uchochezi, kejeli, matusi kwa vongozi wa Serikali waliopo madarakani na Serikali kwa ujumla zinazoweza kusababisha kutendeka kwa vitendo vya uvunjifu wa amani.

“Maandamano hayo yasisababishe uvunjifu wa amani, watu kuporwa, watu kuibiwa au kuharibiwa mali zao. Mnaelekezwa kupita kwenye barabara mlizoomba kupita,” imesema taarifa.

Aidha, amewakumbusha kuwa katika makutano ya barabara za Kenyata na Nyerere, viongozi na waandamanaji hawatoruhusiwa kufanya mkutano wa hadhara mahali hapo hadi watakapofika uwanja wa Furahisha pamoja na kutumia upande mmoja wa barabara ili kuwapa nafasi watumiaji wengine wa barabara kuendelea na shughuli zao.

Imeongeza kuwa ukiukwaji wowote utakaofanyika utalazimisha Jeshi la Polisi kuchukua hatua za kisheria ili kuzuia uvunjifu wa amani.