
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imeitaka Klabu ya Yanga irudishe kwenye mfuko wa klabu TZS milioni 100 iliyokichangia Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu.
CHADEMA imesema kuwa hatua hiyo itaonesha kuwaheshimu wanachama na mashabiki wanaochangia klabu hiyo na wanaounga mkono vyama vingine vya siasa.
Taarifa iliyotolewa na CHADEMA imesema kitendo cha Yanga kuichangia CCC ni kuwadharau mashabiki wake, pia kinakiuka kanuni za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) ambalo linakataza vilabu kujihusisha na siasa.
“CHADEMA tunaitaka Yanga kujiepusha na siasa kwa namna yoyote ili kuhakikisha kuwa michezo inabaki kuwa jukwaa la umoja na kuwaunganisha watu na si chombo cha kuwagawa wananchi,” imesema.
Aidha, CHADEMA imeenda mbali zaidi na kusema kuwa taarifa iliyotolewa na klabu hiyo kwamba pesa hizo zimetoka taasisi ya GSM inalenga kuwahadaa wananchi.








