CHADEMA yakubali mdahalo na Makonda, yatoa masharti

0
26

Baada ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda kutoa rai kwa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufanyike mdahalo baina ya viongozi wa CHADEMA pamoja na yeye kabla ya kufanyika kwa maandamano Januari 24, chama hicho kimesema kiko tayari kukutana na kujadili.

CHADEMA imesema “msimamo wa chama ni kuwa kama anataka mdahalo sisi kama chama tupo tayari na hatujawahi kukimbia midahalo kama wao na chama chao.”

CHADEMA imependekeza mdahalo huo ufanyike katika maeneo mbalimbali moja wapo ni Serikali kuondoa miswada mitatu bungeni ili kuwezesha wadau mbalimbali kukaa kwenye mdahalo wa kujadili maudhui ya Miswada ya Sheria za Uchaguzi, Tume ya Uchaguzi na Sheria zinazohusu masuala ya vyama vya siasa.

Jambo la pili ni Serikali kuanzisha mara moja mchakato wa marekebisho ya Katiba ya mwaka 1977 ili kuwezesha kuondoa mapungufu yaliyomo kwenye Katiba hiyo ili kuruhusu maandalizi ya kuandikwa kwa miswada mipya ya kuboresha mifumo ya uchaguzi nchini.

Tatu, Serikali iwasilishe bungeni muswada wa sheria ya kusimamia uchaguzi wa Serikali za mitaa na uchaguzi huo usimamiwe na tume ya uchaguzi badala ya TAMISEMI.

Pia, Serikali iwasilishe muswada wa sheria wa kukwamua mchakato wa Katiba Mpya ukiwa na mwelekeo.

“Wadau tutaweza kukaa kwenye mdahalo ili kuishauri Serikali jinsi ya kuweza kupunguza ukali wa gharama za maisha na kuonyesha kodi na tozo zipi zipunguzwe, anasa gani ziondolewe Serikalini na mkakati mzima wa kupunguza ukali wa gharama za maisha kwa wananchi,” imeeleza CHADEMA

Aidha, CHADEMA imemtaka Makonda kuweka mdahalo na Serikali ili kuona ulazima wa kusikiliza na kuheshimu maoni ya wananchi na wadau mbalimbali wa chaguzi katika kuandaa mazingira bora ya kuwa na chaguzi huru na haki.

Send this to a friend