CHADEMA yapinga deni la TPDC na TANESCO kuwa deni la taifa

0
15

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimepinga suala la Wizara ya Nishati kuhamisha madeni ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutoka kwenye vitabu vya mashirika hayo kwenda kuwa deni la taifa.

Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ambaye pia ni mshauri wa chama katika uchumi na fedha, Ahobokile Mwaitenda wakati akizungumza na waandisi wa habari leo Desemba 5, 2022.

Amesema kauli ya Waziri wa Nishati, January Makamba iliyonukuliwa katika gazeti la The Citizen kuhusu jumla ya deni la TZS trilioni 5 kuhamishwa kuwa deni la Serikali ilijaribu kushawishi umma kuwa hakuna madhara yoyote kufanya hivyo jambo ambalo si kweli.

Rais Samia aagiza milioni 960 za uhuru zijenge mabweni

“Deni la Serikali ambalo linalipwa na Serikali ni lile deni linalokopwa na Serikali lakini hili deni lingelipwa na TANESCO na TPDC wala kodi zetu na tozo zetu zisingehusika humo,” amesema.

Aidha, amesema Serikali haijatoa sababu za mashirika hayo TPDC na TANESCO kushindwa kulipa madeni hayo na ni hatua gani zilizochukuliwa ikiwemo uajibishwaji baada ya kushindwa kulipa deni hilo.